Questo sito utilizza cookies tecnici (necessari) e analitici.
Proseguendo nella navigazione accetti l'utilizzo dei cookies.

Franz Cerami anaeleza sura ya kibinadamu ya mnyororo wa thamani wa kahawa nchini Kenya

Nairobi, 2 Juni 2026 — Katika maadhimisho ya Siku ya Jamhuri ya Italia, Makazi ya Balozi wa Italia jijini Nairobi yanaandaa Jute Portraits, mradi mpya wa kisanaa wa Franz Cerami, uliotekelezwa kwa mpango wa Ubalozi wa Italia nchini Kenya, kwa ushirikiano na Taasisi ya Utamaduni ya Italia jijini Nairobi pamoja na mpango wa ACT Coffee wa UNIDO (Advancing Climate-Resilience and Transformation in African Coffee).

Mpango wa ACT Coffee ni mpango wa kimkakati unaoungwa mkono na Ushirikiano wa Maendeleo wa Italia, ndani ya mfumo wa Mpango wa Mattei wa Italia na mkakati wa Ulaya wa Global Gateway. Mpango huu unasaidia nchi za Afrika zinazozalisha kahawa kufanikisha mageuzi ya kimuundo katika sekta ya kahawa, kwa kuimarisha uendelevu wa kijamii na kiuchumi pamoja na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika mnyororo mzima wa thamani — kuanzia kwa uzalishaji hadi usafirishaji wa kahawa nje ya nchi — huku ukiwasaidia wazalishaji na taasisi kukabiliana na mabadiliko ya soko na mahitaji mapya ya kisheria.

Jute Portraits ulizaliwa kutokana na kukutana na wafanyakazi wa mnyororo wa thamani wa kahawa nchini Kenya. Kupitia takriban picha za video 300, msanii anatunga simulizi kuhusu nyuso, ishara, mandhari na hadithi za watu wanaohusika katika uzalishaji wa kahawa: wakulima, wavunaji, wafanyakazi, jamii na maeneo mbalimbali.

Mpango wa ACT Coffee uliundwa mahsusi kubadili hali hii: kuwarudisha watu ndani ya sekta ya kahawa kupitia mafunzo, ujumuishaji wa kiuchumi na utetezi. Kahawa ilizaliwa Afrika. Inalimwa, inavunwa, inasindikwa na kuuzwa na jamii za Kiafrika ambazo kazi yao inaendeleza sekta nzima ya kimataifa — lakini nyuso na hadithi zao husimuliwa mara chache. Nyuma ya kila kikombe cha kahawa kuna mnyororo tata wa thamani unaohusisha sekta nyingi na maelfu ya watu. Jute Portraits inaifanya hadithi hiyo ionekane.

Mradi huu unaunganisha video, uchoraji wa kidijitali, kazi za mikono, grafiti, rangi na vifaa vya asili. Picha zilizorekodiwa nchini Kenya baadaye zinachakatwa tena na msanii kupitia uchoraji wa fremu kwa fremu, na kubadilishwa kuwa picha zinazotembea ambazo zitaoneshwa kwenye majengo mbalimbali ya Nairobi na tarehe 2 Juni ndani ya bustani za Makazi ya Balozi wa Italia.

Kwa ajili ya maonesho hayo, miundo mikubwa iliyotengenezwa kwa mianzi, kamba na gunia la katani iliundwa na msanii kwa ushirikiano na mafundi wa eneo hilo. Katani — nyenzo inayohusishwa kwa namna ya kiishara na usafirishaji na kumbukumbu ya kahawa — hivyo inakuwa sehemu ya uchoraji, uso wa kuoneshea picha na nyenzo hai ndani ya kazi yenyewe.

Mbali na maonesho makubwa ya video, mradi huu pia unajumuisha kazi za sanaa zilizochapishwa kwenye katani, baadhi yake zikitarajiwa kuwa sehemu ya makusanyo ya taasisi mbalimbali nchini Kenya, ikiwemo Ubalozi wa Italia jijini Nairobi, Taasisi ya Utamaduni ya Italia, Makavazi ya Kitaifa ya Kenya na Ofisi ya Umoja wa Mataifa jijini Nairobi.

Maabara ya Visual Storytelling: Vipaji vya Vijana wa Afrika Mbele

Moja ya vipengele muhimu zaidi vya mradi huu ni Visual Storytelling Lab Nairobi, mpango wa mafunzo na ushirikishaji katika uzalishaji uliyoendeshwa sambamba na uundaji wa kazi hiyo ya sanaa.

Maabara hiyo iliwakusanya vijana wabunifu wa Kenya — wapiga picha, watengenezaji filamu na wasimulizi wa hadithi za kuona — katika warsha maalum ya siku mbili iliyoongozwa na Franz Cerami. Mpango huo ulijikita katika upigaji picha za nyuso, simulizi za maeneo, maadili ya matumizi ya picha na mbinu za uzalishaji.

Baada ya warsha, kundi dogo la washiriki waliodhihirisha uwezo mkubwa lilichaguliwa na kuajiriwa kama wasaidizi wanaolipwa kufanya kazi moja kwa moja na Franz Cerami katika hatua zote za uzalishaji wa maonesho hayo: kuanzia kutafuta maeneo ya kurekodia, vipindi vya upigaji picha, uchaguzi wa picha, kurekodi matukio ya nyuma ya pazia hadi hatua za mwisho za maonesho ya picha.

Hiki si kipengele cha pembeni cha mradi huu, bali ya kuwa ni moja kati ya nguzo zake kuu — ni uthibitisho wa dhamira ya mpango wa ACT Coffee katika kukuza ujuzi na uwezo wa kitaalamu wa ndani: kuwafundisha vijana wa Afrika ndani ya mazingira halisi ya uzalishaji wa ubunifu wa kiwango cha juu, wakiwa na majukumu wazi, malipo ya haki na fursa ya kushiriki moja kwa moja katika mchakato wa kimataifa wa kisanaa.

Jute Portraits ilizaliwa kutokana na kukutana na watu wanaofanya kazi katika mnyororo wa thamani wa kahawa nchini Kenya. Niliona nyuso, mikono, ishara, mandhari na simulizi. Kutokana na mikutano hiyo, nilitengeneza picha ambazo nilizichora kwa mkono, fremu baada ya fremu, na kuzigeuza kuwa picha zinazotembea. Kwangu mimi, kazi hii ni njia ya kurejesha hadhi, rangi na uwepo kwa jamii inayochangia kila siku katika historia ya kiuchumi, kitamaduni na kibinadamu inayounganisha Kenya na Italia.”

Franz Cerami

Kupitia Jute Portraits, Franz Cerami anaendelea na utafiti wake wa kisanaa kuhusu uhusiano kati ya miji, jamii na picha za watu. Baada ya miradi iliyotekelezwa katika mazingira mbalimbali duniani, msanii huyo analeta kazi inayounganisha sanaa ya kisasa, diplomasia ya kitamaduni, ushirikiano wa kimataifa na kumbukumbu za maeneo Nairobi.

Maonesho hayo yanathibitisha nafasi ya sanaa kama chombo cha kuunganisha tamaduni, jamii na taasisi.

 

Kuhusu Msanii

Franz Cerami (Naples, 1963) anaishi na kufanya kazi kati ya Naples na Rio de Janeiro. Ni msanii, mwandishi na mhadhiri wa chuo kikuu, na ameteuliwa mara tatu kuwa Balozi wa Ubunifu wa Italia Duniani na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia.

Utafiti wake wa kisanaa unajikita katika matumizi ya mwanga, simulizi za kidijitali na maonesho ya sanaa ya umma. Kazi zake zimewasilishwa katika nchi mbalimbali ikiwemo Italia, Brazil, Armenia, Japan, India, Latvia na Montenegro.

Miongoni mwa miradi yake maarufu ni Lighting Flowers, Red Venus kwa ajili ya MANN – Makumbusho ya Taifa ya Akiolojia ya Napoli, Lumina huko Sarajevo, Remix Portraits huko São Paulo na Yerevan, pamoja na T2 Portraits kwa ajili Uwanja wa Ndege wa Milano Malpensa.

Kwa maelezo zaidi: franzcerami.com .

Gundua zaidi kuhusu Jute Portraits

Jute Portraits - Franz Cerami - Nairobi